(Yohana 4, Matendo 1, 1 Wakorintho 12)
Somo hili limetafsiriwa
kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko
yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978,
1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu
kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa
Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi
(kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu
nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya
kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza
kulipata kwa kubofya kwenye
www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Inamaanisha nini “kubatizwa” kwa Roho Mtakatifu?
Nilipobatizwa, mchungaji alisema “nakubatiza kwa jina la Baba, Mwana na Roho
Mtakatifu.” Je, hiyo inakamilisha jukumu? Kinachonishangaza juu ya jambo hili ni
kwamba watu wengi wanabatizwa kwa maneno hayo hayo, lakini hawaonekani kujawa
sana na Roho katika uzoefu wao wa kidini. Hebu tuzame kwenye somo letu la
Biblia ili tujifunze zaidi!
I.
Kubatizwa Bila Roho Mtakatifu
A.
Soma Luka 1:41-44. Elisabeti ni mama wa Yohana
Mbatizaji. Mariamu ni mama wa Yesu. Habari hii inazungumzia nini juu ya
Elisabeti na Roho Mtakatifu? (Roho Mtakatifu alimjaa Elisabeti, na akaonekana
kumjaa Yohana akingali tumboni kwa sababu Yohana “aliruka kwa shangwe” baada ya
kusikika kwa sauti ya mama wa Yesu.)
B.
Soma Marko 1:4-8. Kwa nini Yohana Mbatizaji
hakubatiza kwa Roho Mtakatifu? Mama yake alijawa Roho Mtakatifu, na inaonekana
Yohana Mbatizaji pia alijawa Roho Mtakatifu hata kabla hajazaliwa.
1.
Yohana Mbatizaji alisema kuwa nani atawabatiza
watu kwa Roho Mtakatifu? (Yesu.)
2.
Angalia tena Marko 1:8. Inawezekana kuwa Yohana
alibatiza kwa maji na Roho Mtakatifu kwa wakati mmoja?
C.
Soma Yohana 4:1-2. Je, Yesu aliwabatiza watu kwa
Roho Mtakatifu? (Hii inaashiria kuwa Yesu hakumbatiza mtu yeyote moja kwa moja.
Lakini, muhimu zaidi ni kwamba, kifungu hakizungumzii jambo lolote kuhusu
wanafunzi, chini ya maelekezo ya Yesu, wakibatiza katika jina la Yesu Kristo.)
D.
Soma Matendo 1:4-5. Hii inatufundisha nini
kuhusu wanafunzi kubatiza katika jina la Roho Mtakatifu au wao kubatizwa katika
jina la Roho Mtakatifu? (Kifungu hiki kinadhihirisha kuwa bado wanafunzi
walikuwa hawajabatizwa kwa Roho Mtakatifu. Kwa kuwa Yesu anarejea tukio la siku
za usoni, inaonekana wazi kwamba si wanafunzi wala wala watu waliowabatiza
walikuwa wamebatizwa kwa Roho Mtakatifu.)
1.
Je, Yohana Mbatizaji ni nabii wa uongo katika
jambo hili? Au, je, Yohana anarejea jambo jingine tofauti anaposema kuwa Yesu “atawabatiza
kwa Roho Mtakatifu” (Marko 1:8)?
2.
Soma Luka 24:49. Yesu anapowaahidi wanafunzi
wake katika Matendo 1:4-5 kwamba “atawapelekea” ubatizo wa Roho Mtakatifu, je,
hiyo ilitimiza unabii wa Yohana Mbatizaji?
3.
Sasa jambo la muhimu kwetu leo – jambo hili
linazungumzia nini kuhusu endapo ubatizo wa maji pia ni ubatizo wa Roho
Mtakatifu? (Hii inatuambia kuwa sio lazima vifanane. Kwa dhahiri havikutendeka
katika kipindi cha maisha ya Yesu hapa duniani.)
E.
Kimsingi hatujui maneno yaliyotumiwa na
wanafunzi wa Yesu katika kuwabatiza watu wakati Yesu alipokuwepo hapa duniani. Ikiwa
walitumia maneno “katika jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu,” basi hiyo
itakuwa wazi kabisa hilo lilikuwa jambo tofauti na kubatizwa katika Roho
Mtakatifu. Hebu tusome Yohana 3:3-8. Je, Yesu alifahamu, katika kipindi cha
huduma yake, kwamba ubatizo wa Roho Mtakatifu ulikuwa muhimu? (Ndiyo!)
1.
Ikiwa Yesu alidhani hivyo, je, ilikuwa na mantiki
kwa Yesu kuwaelekeza wanafunzi wake kubatiza katika jina la Roho Mtakatifu
wakati bado akiwepo hapa duniani?
F.
Soma Mathayo 28:18-20. Soma vifungu hivi kwa
makini. Vinaashiria nini kuhusu endapo wanafunzi wa Yesu walikuwa wakibatiza
katika jina la Roho Mtakatifu hapo awali? (Kauli ya Yesu, ambayo ilitolewa
baada ya kufufuka kwake, ina ushawishi mkubwa katika jambo hili. Yesu anasema
kuwa “nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni.” Matumizi ya
maneno, “basi enendeni” yanaashiria kwamba ni kuanzia katika hatua hii pekee
ubatizo katika jina la Roho Mtakatifu uliidhinishwa. Hii inaonesha kuwa Yohana
Mbatizaji alitabiri kwa usahihi tukio hili, na inaonesha kuwa ubatizo katika
jina la Roho Mtakatifu haukuanza hadi baada ya Yesu kuondoka na kurejea
mbinguni. Kwa dhahiri hii inatusaidia kuelewa Matendo 1:4-5.)
1.
Je, kuna mantiki yoyote katika kungojea muda
huu? (Soma Warumi 6:3-4. Ubatizo haukutimiza maana yake halisi hadi Yesu
alipokufa na kufufuka. Tunapobatizwa majini, tunashiriki katika kifo na ufufuo
wa Yesu. Tunakufa pamoja naye kwa ajili ya dhambi zetu. Hii inaandaa mazingira
ya sisi kujawa na Roho Mtakatifu. Angalia Warumi 8:3-4. Hii ni sehemu ya “mamlaka”
aliyopewa Yesu baada ya kufufuka kwake!)
II.
Filipo na Ubatizo wa Roho Mtakatifu
A.
Soma Matendo 8:5-8. Je, Filipo amejaa uwezo wa
Roho Mtakatifu?
B.
Hebu turuke mafungu kadhaa. Soma Matendo
8:12-13. Nini maoni yako: je, watu wanabatizwa na Filipo kwa Roho Mtakatifu?
C.
Soma Matendo 8:14-17. Unaelezeaje jambo hili? Kwa
dhahiri Filipo amejawa Roho Mtakatifu, lakini bado habatizi katika jina la Roho
Mtakatifu?
1.
Watu hawa “walibatizwaje” kwa Roho Mtakatifu?
(Haukuwa ubatizo. Badala yake, Petro na Yohana kwanza “waliwaombea ili wampokee
Roho Mtakatifu” na kisha “wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho
Mtakatifu.”)
D.
Hebu tupitie chanzo cha tatizo. Soma tena
Matendo 8:15-16. Hii inaashiria kuwa jambo gani halikwenda vizuri? (Jinsi
tatizo lilivyoelezwa inafanya ionekane kwamba ubatizo wa Roho Mtakatifu
unatakiwa ufanyike wakati ule ule ubatizo wa maji unapofanyika. Hiyo ndio
kanuni.)
1.
Utagundua kwamba watu waliweza kuona kuwa bado
Roho Mtakatifu alikuwa hajawajia wakati wa ubatizo. Waliwezaje kutambua hivyo? Unapoona
ubatizo leo, je, unaweza kuelezea juu ya uwepo wa Roho Mtakatifu?
III.
Uthibitisho wa Ubatizo wa Roho Mtakatifu?
A.
Soma Waefeso 5:17-20. Je, unaona ni jambo la
ajabu kwamba Paulo analinganisha ulevi na kujawa Roho Mtakatifu? Kwa nini
asilinganishe mauaji, tamaa, uzinzi au wizi, na kujawa Roho Mtakatifu?
B.
Soma Matendo 2:14-17. Kwa nini Petro anaelezea
katika tukio la Pentekoste kwamba wanafunzi hawajalewa? Kwa nini ulinganifu ule
ule wa ulevi na kujawa Roho Mtakatifu?
1.
Unajuaje kwamba mtu amelewa? (Ulevi unaathiri
uwezo wa mtu kuzungumza na matendo yake yote. Jambo hilo hilo linadhihirika kwa
kujawa Roho Mtakatifu!)
C.
Soma Matendo 19:1-4. Hiki ni kisa kinachofanana.
Je, asili ya ubatizo wao iko wazi? (Ndiyo. Ni ubatizo wa toba wa Yohana
Mbatizaji. Hata hawafahamu habari za Roho Mtakatifu.)
D.
Soma Matendo 19:5-7. Je, wanaume hawa
walibatizwa upya, au Paulo aliweka tu mikono yake juu yao?
1.
Tuna uthibitisho gani kwamba walijawa Roho
Mtakatifu? (“Walinena kwa lugha na kutabiri.”)
E.
Soma Matendo 7:55, Luka 1:67, Matendo 2:4, Matendo
4:31 na Matendo 13:52. Tunaona uthibitisho gani wa kujazwa Roho Mtakatifu katika
hivi vifungu? (Tunaona maono, unabii, kunena kwa lugha, kupeleka injili kwa
ujasiri, na kujaa furaha.)
F.
Soma 1 Wakorintho 12:4-7. Jambo gani linatolewa “kwa
manufaa ya wote?” (Ufunuo wa Roho Mtakatifu.)
Je, “kumdhihirisha” Roho Mtakatifu ni sawa na “kujawa” Roho Mtakatifu? (Nadhani. Kama sio sawa kabisa, basi vinaonekana kukaribiana sana. Kama “umejawa” unapaswa “kudhihirisha.”)
G.
Soma 1 Wakorintho 12:8-11. Tunawezaje kufahamu
kwamba tumebatizwa kwa usahihi kwa Roho Mtakatifu? Tunawezaje kufahamu kwamba
tumejawa Roho Mtakatifu? (Tutadhihirisha mojawapo au nyingi ya hizi karama za
roho.)
1.
Sitakuhitaji usome vifungu sasa hivi, lakini
kuna hoja zinazojengwa juu ya vifungu vya Agano Jipya kwamba uthibitisho wa
kujawa Roho Mtakatifu ni kuwa na uwezo wa kunena kwa lugha. Kunena kwa lugha ni
miongoni mwa karama zilizoorodheshwa ambazo tumezisoma. Je, 1 Wakorintho 12:11
inatufundisha nini juu ya hii hoja? (Inasema kuwa karama za roho, kama vile
kunena kwa lugha, zinatolewa na Roho Mtakatifu, “kama apendavyo yeye.” Hiyo inamaanisha
kuwa si wote tutakaokuwa na karama inayofanana.)
2.
Sasa swali gumu: je, umedhihirisha mojawapo kati
ya hizi karama za roho? Angalia orodha kwa makini kabla hujajibu.
H.
Rafiki, ikiwa huna uhakika kama umejawa na Roho
Mtakatifu, kwa nini usimwombe mtu aliyejawa Roho Mtakatifu akuwekee mikono ili
kutatua tatizo hilo? Kama bado hujabatizwa, kwa nini usiombe kubatizwa katika
jina la “Baba, Mwana na Roho Mtakatifu?”
IV. Juma lijalo: Roho Mtakatifu na Kuishi Maisha Matakatifu.

No comments:
Post a Comment